All releases
Coat of arms of Uganda
Uganda Media Centre · Official Record Reference: UMC/VYOMBO-VYA-HABARI-MUHIMU-KATIKA-KUKIKUZA-KISWAHILI-UGANDA-21ZB/20260811

Command Centre / Press Room / Social

Social

Tuesday, 11 August 2026 · 4 min read

VYOMBO VYA HABARI MUHIMU KATIKA KUKIKUZA KISWAHILI UGANDA

VYOMBO VYA HABARI MUHIMU KATIKA KUKIKUZA KISWAHILI UGANDA

Na Monday Akol Amazima

Tarehe 7, Julai 2026, wakati ulimwengu na walimwengu walipokuwa wanasherekea maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani (MASIKIDU) Waziri wa TEHAMA na Kuongoza Taifa wa Uganda Mhe. Justine Kasule Lumumba alijiunga na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Habari Uganda Bw. Alan Kasujja kuzindua Dawati la Kiswahili. Dawati hilo litakuwa na jukumu la kuratibu maendeleo ya Kiswahili katika vyombo vya habari nchini Uganda.

‘Wakati umewadia vyombo vya habari kuwa sehemu ya mpango wa serikali kukienzi Kiswahili’ alisema Bw. Alan Kasujja. Uzinduzi huu ni hatua kubwa katika kuendeleza Kiswahili katika tasnia ya habari nchini Uganda kwa vile dawati hili pia litashughulikia mawasiliano ya serikali kwa umma katika Kiswahili.

Ukosefu wa Kiswahili katika mawasiliano ya serikali nchini Uganda kwa umma ilikuwa changamoto kubwa huku wengi wakihisi hakuna utashi wa kisiasa katika kueneza Kiswahili. Na kweli utashi wa kisiasa ni nguzo kubwa katika kueneza jambo lolote lile.

Hapo awali mara nyingi Kiswahili kilipotajwa, baadhi ya Wanauganda walihisi kuwa ni lugha ya kufundishwa katika baadhi ya shule, lugha ya wahuni na au lugha ya jeshi. Ukweli ni kuwa taswira ya Kiswahili Uganda inaendelea kubadilika na kuwa nzuri. Ingawa Uganda imepiga hatua katika kuendeleza Kiswahili hasa katika tasnia ya elimu kiasi kwamba sasa Kiswahili ni somo la lazima kwa kidato cha kwanza na cha pili, bado kuna pengo kubwa katika tasnia ya habari.

Kuna kila haja ya kuwezesha vyombo vya habari na waandishi habari kuwa sehemu ya uenezaji wa Kiswahili Uganda na kwingineko. Kulingana na takwimu kutoka Tume ya Mawasiliano Uganda yaani Uganda Communications Commission, Uganda ina vituo 54 vya televisheni.

Jambo la kushangaza ni kuwa ni vituo 4 tu vinavyotoa huduma kwa Kiswahili. Vile vile Uganda ina zaidi ya vituo vya redio 278, ila ni kama vituo 30 vinavyotoa matangazo katika Kiswahili. Na kwa upande wa gazeti au jarida tunaweza kusema hakuna kwa vile majarida na gazeti vilivyoanzishwa bado havijapata mizizi tabithi kuendelea.

Kwa hiyo Bw. Alan Kasujja kuanzisha Dawati la Kiswahili ameweka msingi imara kwa uratibu wa maendelo ya Kiswahili katika vyombo vya habari Uganda. Kituo cha Habari Uganda kimeitikia na kusikiliza kilio cha waandishi habari za Kiswahili cha muda mrefu cha kuwepo kituo maalum cha kuratibu kazi yao. Changamoto za waandishi habari za Kiswahili Uganda ni nyingi na dawati hili litakuwa sehemu maalum itakayoshughulikia changamoto hizi.

Katika harakati za kukikuza Kiswahili kama lugha rasmi ya pili Uganda, lugha ya Jumuiya Afrika Mashariki na lugha ya mawasiliano mapana barani Afrika lazima vyombo vya habari vihamasishwe na vihamasike kuhamasisha hadhira yake kukienzi. Waandishi habari pamoja na kuhabarisha umma, wao ndio walimu na kioo cha jamii.

Kwa mantiki hiyo, kama walimu wa umma lazima waelewe umuhimu wa Kiswahili na vilevile namna ya kutumia Kiswahili safi kama chombo cha mawasiliano miongoni mwa watu wa makabila tofauti si Uganda tu bali barani Afrika. Vyombo vya habari huchangia pakubwa kwa kiwango cha lugha (kisarufi) inayozungumzwa na jamii. Kwa hiyo ni muhimu waandishi habari wawe na uelewa tosha wa lugha hiyo. Waandishi habari wanapotumia lugha vibaya, huathiri namna watu wa kawaida watakavyotumia lugha hiyo.

Tofauti na Tanzania na Kenya ambapo kuna asasi na vituo vingi vya kuwakosoa na kuwanoa waandishi habari za Kiswahili ili waweze kutumia lugha kwa ufasaha, nchini Uganda kumekuwa na pengo hili kwa muda mrefu. Na uanzishaji wa dawati hili ndio mwanzo wa safari ya kuratibu matumizi ya Kiswahili safi katika vyombo vya habari Uganda.

Nina imani kuwa waandishi habari na vipindi vya Kiswahili vitaongezeka katika vyombo vya habari Uganda kwa vile sasa mkono wa serikali umeonekana bayani kwa kutaka tasnia ya habari iwe sehemu ya ukuzaji wa Kiswahili.

Uganda inaendelea kupiga hatua katika kukikuza Kiswahili kiasi kuwa kila juma tatu baraza la mawaziri hujifunza Kiswahili. Rais Yoweri Museveni mara kwa mara amewahimiza Wanauganda kujifunza Kiswahili kuashiria uhuru wa Mwafrika. Na kweli baadhi ya wizara na mashirika ya serikali wameitikia wito wake kwa kuanzisha mafunzo ya Kiswahili kwa watumishi wake.

Mbali na Rais Museveni, Mkuu wa Jeshi la Uganda People’s Defence Force, Jenerali Muhoozi Kainerugaba pamoja na kuwa mkereketwa wa Kiswahili, operesheni nyingi za kazi yake amezipatia jina la Kiswahili. Kwa mfano siku hizi vita aliyoanzisha dhidi ya ufisadi imepewa jina operesheni ondoa ufisadi. Vile vile hata katika maongezi yake kwa Kiingereza si rahisi kuhitimisha ujumbe wake bila kuweka maneno ya Kiswahili.

Mwisho ingawa sio kwa umuhimu, Kituo cha Habari Uganda kinahitaji kila aina ya msaada kutoka kwa wadau wote wa Kiswahili kiweze kutimiza ndoto ya kueneza matumizi ya Kiswahili katika tasnia ya habari. Kwa hiyo asasi za lugha na habari katika nchi zilizopiga hatua ya kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika vyombo vya habari kama Tanzania na Kenya, zitakuwa msaada mkubwa sana kwa dawati hili.

Mwandishi ni Mkuu wa Dawati la Kiswahili la Kituo cha Habari Uganda